Maswali na Majibu Kuhusu Sayari na Nyota

Ufahamu kuhusu sayari unafundishwa katika ngazi ya shule ya msingi na sekondari nchini Tanzania. Walimu, wanafunzi na wazazi wanaweza kudhani kuwa wanaufahamu wa kutosha kuhusu sayari. Hata hivyo, kipindi cha macho angani kuhusu sayari bado kimeibua maswali na udadi zaidi juu ya ufahamu kuhusu sayari. 

Yafuatayo ni baadhi ya maswali na majibu kuhusu sayari yaliyoulizwa na wanafunzi kutoka shule ya msingi Ilboru kwa kushirikiana na mwalimu wao Eliatosha Maleko na kujibiwa na Mchungaji Ingo Koll aliyeanza kwa kusema.

“Vijana wapendwa katika klabu ya sayansi, nimepokea maswali yenu. Asanteni sana! Basi hapa majibu yangu!”

 1. Maliki Abasi aliuliza:  Kwanini Sayari zote haziwezi kuonekana kwa wakati mmoja kama zinavyooneka baadhi ya Sayari kama vile Jupiter, Saturn , Mars, na Venusi  wakati huu? Nini sababu ya msingi?.

Jibu: Kama ungeweza kupanda chombo cha anga nje na kwenda mbali kidogo katika anga-nje, ungeweza kuona sayari zote kwa wakati moja. Ila tukiwa duniani, hatuwezi. Kwanza Sayari hazikai mahali pamoja. Kila sayari inazunguka Jua kwa kasi yake tofauti na kwa umbali mkubwa kati yake. Pili  tunaona nusu ya anga tu, nusu nyingine hatuioni, inaonekana  upande mwingine wa Dunia. Tatu wakati Sayari iko upande mwingine wa Jua, hatuioni. 

2. Neema Florence aliuza: Ni kwanini Sayari hazitoi  nuru yake pekee yake na kutegemea nuru itokanayo na Nyota ya jua?

Jibu: Asante Florence, swali lako ni zuri lakini halihusu sayari pekee. Kwa nini kuna vitu vinavyotoa nuru lakini vingine ambavyo ni vingi vinaakisi nuru tu?Hapa Dunaini ni vitu gani vinavyotoa nuru? Mshumaa, balbu katika taa na Moto. Vitu vyote vingine havitoi nuru, vinaakisi tu. Hali hiyo tunaona tukizima taa usiku. Kuna giza. Tukjiwasha tunaona vitu ambavyo vinaakisia nuru ya taa.

Jua pamoja na nyota kwa jumla ni magimba yanayotoa nuru. Sayari ni magimba ambayo hayana nuru yenyewe, yanaakisi nuru,

Tofati kuu ni, ndani ya nyota kuna mabadiliko ambamo atomu zinapasuliwa na kuunganishwa upya. Katika kazi hii nishati nyingi inaachishwa. Sehemu ya nishati hiyo tunaona kama nuru.

Kwenye sayari mabadiliko hayo hayatokei kwa sababu ni ndogo. Unahitaji masi kubwa sana ili nguvu ya graviti igandamize atomu kiasi cha kwamba zianze kuachana na kuungana upya.  

 3.Clara aliuliza: Tunaelewa kuwa Sayari pekee ambayo ni dunia ndio Sayari pekee ambamo viumbe hai mbalimbali hupatikana humo, Je katika Sayari nyingine hasa zile zilizokaribu na jua wanasayansi hawajawahi kutoa majibu ya uwezekano wa kuwa na viumbe hai kama ilivyo katika Sayari ya dunia?.

Jibu: Kwa elimu tuliyo nayo sasa inaeleweka kwamba Dunia ni sayari ya pekee penye uhai kama tunaoufahamu. Utaridi (Mercury) iko karibu na Jua, kuna mnururisho mkali kutoka kwenye Jua, hakuna angahewa, joto upande wa mchana yaani upande unapotazama Jua ni kali. Vivo hivyo baridi kwa upande wa usiku ni kali. Hivyo hakuna uhai unaweza kudumu huko.

Zuhuru (Venus) ina joto la kudumu la zaidi ya nyuzi 400 kote. Hakuna uhai unaoweza kudumu huko. Wataalamu walichunguza kama labda kuna uwezekano wa aina ya bakteria wanaoelea kwenye mawingu ya angahewa lakini hilo halikuthibitishwa.

Mirihi (Mars) ina angahewa hafifu mno, karibu hakuna. Tena ni baridi. Magari ya utafiti yaliyopo sasa yanatafuta dalili za uhai, labda bakteria fulani lakini hadi sasa hakuna dalili zilizopatikana; wataalamu wengi huamini hakuna dalili za uhai.

Kuna sehemu moja ambako wataalamu wachache wanataka kufanya utafiti, ambayo ni mwezi mkubwa  wa Zohali unaoitwa Titani. Hata hapa wengi hudhani hamna lakini siku moja kipimaanga kitapelekwa Titani na kufanya vipimo kutambua kama namna sahili ya uhai kama bakteria inaweza kuwepo.

4.Daniel Willfred aliuliza: Tulipokuwa tunasikiliza kipindi tulisikia kuwa nyota zina joto kali sana je ina maana gani je nyota huzalisha joto kutoka wapi ilhali  tumejifunza kuwa SAYARI pamoja na nyota zote zinategemea Jua ili ziweze kuakisi mwanga wake?.

Jibu: Joto la nyota hutoka ndani yake. Jotohutokana na masi kubwa sana ya gesi. Masi hiyo kubwa inajikaza kutokana na nguvu ya mvutano au nguvu ya graviti. Kujikaza kwake kunasababisha shinikizo kali kiasi kwamba atomu zenyewe zinaanza kuachana.

Kila atomu huundwa na chembe ndogo zaidi tunazoiita protoni, nyutroni na elektroni. Kwa kawaida atomu huwa na muundo imara kabisa. Lakini kama inaathiriwa na kani kubwa sana, chembe hizo ndani yake zinaweza kuachana na kuungana upya. Wakati chembe hizo huaachana na kujipanga upya, nishati inaachishwa tunayoona kwa umbo la joto na nuru. 

Kwa sehemu ya sentensi yako hapa hujaelewa sawa. Sayari ni ndogo kuliko Jua na hapa hakuna kuachana kwa atomu ndani yake. Hivyo hazing‘ai hazitoi nuru; zinaakisi mwanga.

Lakini nyota hazipokei mwanga kutoka kwenye Jua, hivyo haziakisi. Kila nyota ni kama Jua letu, mara nyingi kubwa zaidi. Tunaziona kama mianga midogo kwa sababu ziko mbali.    

 Rith Piniel aliuliza: Ni kwanini nyota haibadiliki na kila siku zinakua ni zile zile au kunakuwaga na mabadiliko ya nyota?.

Jibu: Maishani mwetu hatuoni mabadiliko ya nyota kwa macho yetu, isipokuwa kwa kutumia mitambo inayoweza kupima kwa umakini mkubwa.

Nyota zote zinasogea katika anga kuelekea nje, tena kwa kasi tofauti baina yake. Kutokana na umbali mkubwa uliopo hatulihisi hili katika wakati wa maisha yetu. Lakini wajukuu wa wajukuu wetu wataona nyota kwenye nafasi iliyo tofauti na iliyopo leo. Wataona pia nyota ambazo sisi hatuwezi kuona kwa sababu kwa wakati huu zinaonekana kwenye kizio cha kaskazini cha Dunia tu.

 6. Aneth Alistides aliuliza: Je nyota hufa kama viumbe walioko ulimwenguni na zinapokufa huenda wapi? 

Jibu: Maisha na kifo cha nyota ni tofauti sana na maisha na kifo cha viumbe wa duniani maana si viumbe hai. Lakini hata nyota huwa na mwanzo na mwisho. Hapo tunaweza kusema kuna Maisha ya nyota, nyota inazaliwa, nyota inakufa“. 

Mabadiliko hayo hutokea katika ki/vipindi virefu sana vya miaka mabilioni, kwa hiyo hatuwezi kuona mabadiliko hayo katika maisha yetu wala kupata madhara yake. 

Wataalamu wengi hudhani kwamba Jua letu litakufa baada ya miaka bilioni kadhaa.  

Wakati nyota inakufa, yale yanayofuata hutegemeana na ukubwa wake. Nyota kubwa sana hufa katika mlipuko. Inapokufa vitu vilivyomo ndani yake vyote hulipuka na kutawanyika na kusambaa katika uwazi wa anga inayoizunguka. Vipande hivi huelea angani kama wingu, hadi,  baada ya muda mrefu,  vinakamatwa na nguvu ya uvutano au nyota nyingine iliyo karibu, labda na wingu kubwa zaidi ambalo litaanza kuvivuta kwake.

Kwa hiyo  mabaki ya nyota iliyokufa, yanaweza kuwa sehemu ya nyota mpya na sayari zake. 

 Na je nini madhara ya kufa kwa nyota katika maisha ya  mwanadamu au viumbe hai?

Jibu: Kwanza kuna faida ya kufa kwa nyota. Maana miili yetu ina asili katika nyota. Namna gani?

Tumejifunza miili yetu imejengwa na seli. Seli zimejengwa na nini? Tunajua mwili wetu unabadilisha virutubisho tunavyopata katika chakula. Lakini hivi vimeundwa na nini? 

Hapa tunaweza kuwauliza wanakemia ambao watajibu: Seli za mwili na pia chakula tunachokula vimefanywa na molekuli mbalimbali. Molekuli zinaundwa kwa kuunganisha atomu za elementi mbalimbali. Kwa jumla tunajua takribani elementi 90 zinazounda kila kitu, takriban elementi 30 zinajenga miili yetu. Isipokuwa elementi ya haidrojeni, zote nyingine zilizoundwa ndani ya nyota na kusambaa katika ulimwengu kwa njia ya milipuko ya nyota miaka bilioni iliyopita.

Kwa njia hiyo zilifika pia katika wingu la atomu lililoendelea kuwa Jua letu na sayari zetu.

Kutokana na milipuko ya nyota zilizopita elementi hizi zimefika pia duniani na hivyo viliweza kupatikana kwa miili yetu.

Bila kifo cha nyota zilizotangulia tunsingekuwepo.

Upande wa madhara – hilo ni swali pana na la mbali sana. Kifo cha nyota kinaweza kutokea kwa njia ya mlipuko. Tunajua mlipuko wa karibu una hatari.  Kama nyota iliyo karibu ingelipuka, ingeweza kutuathiri. 

Lakini mlipuko wa nyota hautokei mara kwa mara katika mazingira ya Jua letu. Wataalamu wamechungulia nyota zote zinazopatikana katika umbali wa miaka ya nuru 100 – hawakutambua yoyote inayoonyesha dalili za kukaribia mwisho wa maisha yake. Zile ambazo zimetambuliwa kukaribia mwisho ziko mbali mno. 

Uwezekano mkubwa ni: katika miaka mielfu inayokuja, hakuna mlipuko wa nyota inayoweza kuathiri dunia.

 7. Kwanini nyota nyingi hushuka kutoka Magharibi na sio Mashariki  na nikawa ni nini?

Jibu: Naomba swali hili mjibu ninyi wenyewe kwa pamoja! Nitaongeza jibu langu mwishoni kabisa baada ya swali lenu la mwisho.

 8. Emaculata aliuliza: Je nyota zimeundwa na nini? Je zinakuwa na anga lake na ardhi kama ilivyo  katika  Sayari ya dunia?.

Jibu: Nyota ni tofauti na sayari kwa muundo, ukubwa na halijoto. Kila nyota ni gimba kubwa sana la gesi ambayo ina joto sana, halijoto inafikia nyuzi milioni. Gesi ya nyota iko katika hali ya kipekee inayoitwa plazma, au kwa neno  Sababu ya joto ni moto ya pekee inayoendelea mfululizo ndani ya kila nyota, Ni moto ya pekee kwa sababu kila nyota ina sehemu ndani yake ambako atomu zinaachana na kuunganishwa na hapo kuna nishati nyingi inayoachishwa kwa umbo la joto na nuru.

Sayari ni magimba ambayo ni makubwa kwa macho yetu lakini tukilinganisha na nyota ni madogo. Kwa mfano sayari zote kwenye mfumo wa Jua letu ni kama asilimia moja ya masi ya Jua. Kati ya sayari hizo Mshtarii peke yake ina masi kubwa kushinda sayari zote nyingine kwa pamoja.

Ndani ya sayari hakuna moto wa kudumu inaounganisha atomu, hivyo zimepoa.

Sasa naongeza jibu langu kuhusu swali la saba_ 7: Sababu za nyota kushuka magharibi ni sawa na sababu ya Jua kushuka magharibi. Maana hali halisi nyota na Jua hazipandi wala kushuka.

Ziko palepale na maishani mwetu hazibadiliki.

Lakini sisi tunazunguka. Au niseme kikamilifu zaidi: Dunia yetu inajizungusha pamoja nasi tulipo kwenye uso wake.

Upande wa mashariki tunapozungushwa tunaona Jua na nyota hupanda juu ya upeo wa macho. Baada ya saa 12 hivi,  tumepita chini ya nyota na Jua na sasa upeo wa macho wa upande mwingine unakaribia nafasi zilipo. 

Kila kitu kwenye anga kinaonekana kupanda upande wa mashariki na kushuka upande wa magharibi, kwa sababu huo ndio mwelekeo wa mzunguko wa sayari yetu.

 

Leave a Reply